Friday, June 8, 2012

Mapacha walioungana wafariki dunia

WATOTO mapacha walioungana waliozaliwa juzi katika hospitali ya Muhimbili wamefariki dunia usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

Watoto hao walioungana kuanzia kifuani walikuwa na jinsi moja ya kike na miguu miwili, lakini katika eneo la juu walikuwa na vichwa viwili na mikono minne.

Akizungumza ofisini kwake, Daktari bingwa wa watoto, Augustine Massawe alisema watoto hao wamefariki kabla ya kufanyiwa vipimo ambavyo vingeeleza uhusiano mzima wa kimaumbile.

“Hawa ni mapacha walioungana, ni watoto wawili ambao sehemu ya tumbo na kifua havikutengana wakati wa ukuaji akiwa kwenye mfuko wa uzazi, na mara nyingi watoto kama hawa huzaliwa kwa upasuaji,” alisema.

Alieleza kwamba kitaalamu watoto hao huitwa ‘Conjoined twins’ ambao hutengenezwa kwenye mfuko mmja na hutumia kondo moja kwa kila kitu katika kupata mahitaji kutoka mama, pia iwapo wangeendelea kuwa hai pengine wangekuwa na matatizo ya ubongo.

Dk Massawe alisema kuzaliwa kwa watoto wa aina hiyo hakuhusishwi na imani yoyote na si mara kwanza Tanzania kutokea uzao wa aina hiyo kwani kila baada ya mwaka mmoja Hospitali ya Muhimbili hupokea uzazi wa aina hiyo.

Alisema kuwa madaktari walishangazwa na namna mama huyo alivyoweza kujifungua watoto hao kwa njia ya kawaida bila kufanyiwa upasuaji, kitendo ambacho ni nadra sana kutokea.

Alieleza kwamba awali walijua kuwa ni mtoto mmoja kwa mujibu wa vipimo vilivyowasilishwa, lakini wakati wa kujifungua ndipo walipobaini kuwa ni watoto wawili walioungana.

Mama wa watoto hao, Kidawa Mbonde (25) alisema anamshukuru Mungu kwani yote ni mapenzi yake na kwamba kwa sasa anajisikia maumivu makali ya nyonga kuliko kawaida, suala ambalo madaktari wamesema linatokana na kulazimika kujifungua mapacha hao kwa njia ya kawaida.
 http://www.mwananchi.co.tz/habari/3-habari-za-mikoani/23696-mapacha-walioungana-wafariki-dunia

No comments:

Post a Comment