Thursday, April 12, 2012

Watu sita wafa mgodini Mirerani


Joseph Lyimo, Mirerani
WACHIMBAJI wadogo sita wa madini ya Tanzanite katika Mji Mdogo wa Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wamefariki dunia baada ya kudondokewa na pipa la kutolea udongo mgodini (dunganya).

Pipa hilo ambalo hutumika kutoa udongo kutoka chini mgodini, lilikatika ghafla wakati kazi ya kutoa udongo kutoka mgodi huo ikiendelea na kuwaponda wachimbaji hao wadogo ambao walifariki papo hapo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Eurelia Msindai alithibitisha tukio hilo akisema wachimbaji hao walikuwa wafanyakazi wa mgodi unaomilikiwa na Jubilate Olomi mkazi wa Mirerani.

Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 10 saa 1:30 usiku kwenye mgodi huo wa Olomi uliopo Kitalu B (Opec) katika machimbo ya madini ya Tanzanite Mji Mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro.

Kaimu Kamanda Msindai alisema kuwa chanzo cha vifo hivyo ni ajali mgodini akieleza kuwa wachimbaji hao walikuwa wakichota udongo mgodini kutumia pipa hilo ambapo  wakati wakiendelea na kazi pipa hilo lilikatika ghafla na kuwadondokea.

“Ni tukio la bahati mbaya kwani awali walikuwa wakiendelea na kazi vizuri, lakini kifaa kijulikanacho kama XL kinachoendeshea mtambo huo kikakatika na kuwadondokea na kufariki dunia papo hapo,” alisema Msindai.

Aliwataja marehemu hao kuwa ni Haruna Jumanne (24) aliyekuwa mkazi wa Kazamoyo Mirerani, Bakary Shamba (24), mkazi wa Songambele Mirerani, Tumaini Gasper (23), mkazi wa Songambele na  Valerian Raphael (31) mkazi wa Ulong’a Meru mkoani Arusha.

Wengine ni Oscar Olomi (60), mkazi wa Sanja Juu wilayani Siha mkoani Kilimanjaro na Hassan Hussein (30) mkazi wa Songambele Mirerani.

Kaimu Kamanda Msindai alisema miili ya marehemu hao imehifadhiwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru) kwa uchunguzi zaidi na hakuna mtu anayeshikiliwa na polisi kwa kuhusika na tukio hilo.

http://www.mwananchi.co.tz/habari/3-habari-za-mikoani/21950-watu-sita-wafa-mgodini-mirerani

No comments:

Post a Comment