Saturday, April 7, 2012

Ngeleja: Mauzo ya madini yameongeza pato la taifa
Waziri wa Nishati na Madini Wilium Ngeleja
Nora Damian na Patricia Kimelemeta
SERIKALI imesema fedha za mauzo ya madini zimeongezeka kutoka Dola 26.6 milioni za Marekani  hadi  bilioni moja kwa mwaka.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa kuzindua Bodi ya Ushauri wa Madini, Waziri wa Nishati na Madini, Willium Ngeleja alisema,  sekta hiyo imekua kutoka asilimia 7.7 hadi  asilimia 10.7.

Alisema mauzo ya madini nje ya nchi yanaongoza kwa kufikia asilimia 52 ya mauzo yote na kwamba pato la taifa kutokana na sekta hiyo limeongezeka kutoka asilimia 1.4 hadi kufikia asilimia 2.7.

Alisema uchimbaji unaoendelea nchini hivi sasa unafanyika kwa asilimia 10 tu ya rasilimali zilizopo na kwamba kuanzia sasa serikali itakuwa inamiliki hisa katika migodi ya kati na mikubwa.

“Tanzania bado ni nchi changa katika uchimbaji wa madini , hatuna zaidi ya miaka 15 hivyo hatuwezi kujilinganisha na nchi nyingine kama Afrika Kusini ambayo ina zaidi ya miaka 100,”alisema Ngeleja.

Alisema pia wametenga jumla ya hekta laki tano katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini.

Kwa mujibu wa Ngeleja mballi na hekta hizo pia wameanzisha utaratibu wa kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuanzisha vituo vya kuwakopesha na kuwakodishia vitendea kazi.

Alisema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana zaidi ya leseni 27,000 zilikuwa zimetolewa kwa wachimbaji na watafutaji madini huku leseni 20,000 zikitolewa kwa wachimbaji wadogo.

Alisema leseni kwa ajili ya watafutaji wakubwa zilitolewa 6,093 na kwamba muda wa leseni ndogo za madini umeongezwa kutoka miaka mitano hadi saba.

Pia aliongeza  kuwa madini ya vito yatachimbwa na Watanzania pekee isipokuwa kama uchimbaji  huo utahitaji mtaji mkubwa na teknolojia ya kisasa na kwamba wageni wataruhusiwa kuingia ubia  kwa hisa zisizopungua asilimia 50.
Kwa upande wa mikataba alisema , kuanzia sasa itakuwa inapitiwa kila baada ya miaka mitano.

Naye Mwenyekiti wa bodi hiyo yenye wajumbe tisa, Richard Kasesela alitoa ushauri kwa wachimbaji wadogo kuzishirikisha serikali za vijiji ziwe na hisa ili kuondoa mgogoro kwenye eneo husika linalochimbwa.
http://www.mwananchi.co.tz/biashara/-/21797-ngeleja-mauzo-ya-madini-yameongeza-pato-la-taifa

No comments:

Post a Comment