Tuesday, April 10, 2012

Katiba mpya iwe urithi wa JK kwa Watanzania
Rais Jakaya kikwete
TUKIO muhimu pengine kuliko yote katika mchakato wa kupata Katiba mpya unaoendelea hivi sasa nchini ni uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa wiki. Katika uteuzi huo, Rais amewateua wajumbe 30 kutoka pande zote mbili za Muungano kwa mujibu wa sheria, huku akimteua Jaji mstaafu Joseph Warioba kuwa mwenyekiti wake.
 
Hatua hiyo ya Rais imekuja siku chache tangu yafanyike mabadiliko katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba katika Mkutano wa Sita wa Bunge la Kumi mwanzoni mwa mwaka huu. Mabadiliko hayo ambayo kwa mara ya kwanza yalizingatia mapendekezo ya vyama vya upinzani na makundi ya vyama mbalimbali visivyo vya kiserikali pia yaliungwa mkono na Rais mwenyewe, huku yakizua malalamiko kutoka kwa wabunge wa CCM.
 
Pengine siyo muhimu kuchambua kwa kirefu katika safu hii mambo yaliyosababisha wabunge wa chama tawala kwa wingi wao kupinga vifungu kadhaa katika marekebisho hayo, kwani hiyo sasa ni historia. Hata hivyo, tunadhani ni vyema angalao kusema kwa kifupi tu hapa kwamba, marekebisho hayo yalizingatia mapendekezo mengi ya Chadema baada ya viongozi wake kukutana na Rais kwa majadiliano na mashauriano katika nyakati tofauti. Baadhi ya mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo yalisababisha hofu kubwa kwa wabunge hao wa CCM, kwani kwao yalionekana yalikuwa na lengo la kuking’oa chama hicho madarakani.
 
Tumelazimika kufanya majumuisho hayo siyo tu kuonyesha jinsi hali ilivyokuwa tete katika ngazi hiyo ya mchakato huo, bali pia kuonyesha jinsi Rais Kikwete alivyojitoa mhanga ili kuhakikisha mchakato huo unazingatia matakwa na maono ya wananchi wote pasipo kutekwa na chama chochote, kikiwamo chama chake cha CCM.  
 
Ni siri iliyo wazi kwamba dhamira nzuri ya Rais Kikwete ya kuhakikisha mchakato wa Katiba mpya hauchakachuliwi  ingehatarisha Urais wake, kwani ulijitokeza uhasi ndani ya chama chake, huku wabunge wa chama hicho wakishikamana kuikwamisha sheria hiyo ya marekebisho ya Katiba. Sisi kupitia safu hii tulimpongeza Rais Kikwete kwa kuonyesha uzalendo uliotukuka na kwa kuweka mbele maslahi ya taifa kwa lengo la kutafuta mustakabali wa nchi yetu kupitia Katiba itakayopatikana kwa maridhiano na mwafaka wa kitaifa.
 
Tulisema pia kwamba hulka na utamaduni wa Rais  Kikwete wa kutafuta mwafaka kwa kushauriana na kuzungumza na makundi mbalimbali katika jamii katika mambo ya msingi kama kuandika Katiba mpya kamwe visitafsiriwe au kuchukuliwa kama udhaifu kwa upande wake. Ndiyo maana tunasema tena leo kwamba, hatua yake ya kuchagua maridhiano na kukataa kushawishiwa kutumia ubabe katika suala muhimu kama kuandika Katiba mpya lazima ienziwe na kila Mtanzania. Rais asitetereke katika hili na ingefaa afarijike kuona kwamba Katiba mpya itakayopatikana kwa maridhiano na ridhaa ya wananchi wote ndiyo hasa utakuwa urithi wake kwa Watanzania punde atakapomaliza kipindi chake cha uongozi mwaka 2015.
 
Ndiyo maana tumefurahishwa na kuridhishwa na uteuzi wake wa wajumbe wa Tume ya Katiba itakayoongozwa na Jaji Joseph Warioba. Uteuzi huo umewakuna wananchi wengi, kwani siyo tu inaidadi kubwa ya wajumbe wenye rekodi ya utumishi wa umma uliotukuka, bali pia inao wajumbe wengi wasomi na baadhi yao wanaheshimika duniani katika masuala ya siasa na katiba.
 
Sisi tunarudia kumuhakikishia Rais kwamba tuko naye bega kwa bega siyo tu katika kuhakikisha kwamba mchakato wa kupata Katiba mpya unafanikiwa, bali pia katika kutoa ushirikiano na wajumbe wa Tume ya Katiba aliowateua mwishoni mwa wiki. Tunawaasa wajumbe hao wasiisaliti  heshima waliyopewa na umma na wahakikishe kazi hiyo inamalizika katika kipindi cha miezi 18 iliyopangwa pasipo kisingizio chochote. Ni matumaini yetu kwamba wajumbe hao wanatambua kwamba wameteuliwa ili kuratibu maoni ya wananchi, hivyo misimamo yao binafsi haina nafasi katika mchakato huo. Tunawatakia kila la kher
http://www.mwananchi.co.tz/uchambuzi/19-maoni-ya-mhariri/21892-katiba-mpya-iwe-urithi-wa-jk-kwa-watanzania

No comments:

Post a Comment