Saturday, April 28, 2012

Kanisa Moravian watoa misaada kwa albino

KANISA la Moravian Tanzania Usharika wa Mabibo, Dar es Salaam, limetoa msaada wa dawa za ngozi na kutangaza kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 32 wa ulemavu wa ngozi.

Mchungaji wa kanisa hilo, Wilbert  Mwasumbi, alisema wanafunzi waliofadhiliwa ni wale wanaosoma kidato cha tatu na nne sekondari za Yusuph Makamba na Mugabe, Dar es Salaam.

“Msaada huu umetugharimu Sh1 milioni, lakini tukaona tusiishie hapo tuwafadhili kwa masomo wanafunzi 32 wa kidato cha tatu na nne kwenye sekondari mbili za Dar es Salaam,”  alisema Mchungaji Mwasumbi.
Alisema licha ya kumshukuru Mungu, kanisa limekaa na kuona uko umuhimu wa kuwatazama hawa wanaoishi na hali ngumu ya afya kutokana na hali zao kipindi cha jua kali.

“Kanisa kwa kuthamini hali ya binaadamu, lilikaa na kufikiri kitakachompendeza Mungu katika kumsaidia binaadamu, hivyo limeamua kuwaangalia hawa maalbino  kuwapatia dawa za kutibu vidonda wanavyopata hasa kipindi cha jua kali,” alisema Mwasumbi na kuongeza: 

“Kanisa limeona uko umuhimu wa kuinua elimu kwa vijana wanaoelemewa kulipia karo za shule na kutoa kipaumbele kwa kulipia karo zao, ili kufikisha malengo ya vijana kujikomboa kwa maisha, hivyo tumeanza kwa shule hizi mbili na baadaye tutaendelea nyingine.”  

Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Wilaya ya Kaskazini, Mchungaji Alinanuswe Mwakilema, alisema licha ya wao kuwa sehemu ya jamii, iko haja ya kulitambua suala la kuwaangalia maalbino kwa msaada zaidi.
Hata hivyo, Mwakilema alisema hivi karibuni Serikali iliweka ulinzi kwa maalbino kwa kuhakikisha kunakuwapo usalama, lakini hivi sasa umesitishwa.http://www.mwananchi.co.tz/biashara/13-biashara-za-kitaifa/22403-kanisa-moravian-watoa-misaada-kwa-albino

No comments:

Post a Comment