Monday, April 9, 2012

Hatima ya Lulu iko mikononi mwa DPP


Boniface Meena 
HATMA ya msanii maarufu wa kike Elizabeth Michael maarufu kama ‘Lulu’ anayeshikiliwa polisi kufuatia kifo cha msanii Steven Kanumba iko mikononi mwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema suala la msanii huyo kusema ana kesi ya kujibu au la, liko mikononi mwa DDP ambaye ndiye atakayepitia jalada baada ya polisi kukamilisha upelelezi wao.

Kamanda Kenyela alisema Lulu kupelekwa mahakamani ni uamuzi wa DPP ambaye atatakiwa kulipitia faili lake na kujiridhisha kama ana kesi ya kujibu au la.  “Kumpeleka mahakamani ni mpaka DPP tutakapomwasilishia jalada la tuliyoyakusanya na ndiye atakayeamua kama kuna kesi ya kujibu au hakuna,”alisema Kamanda Kenyela.

Alisema hadi hivi sasa bado wanasubiri ripoti ya uchunguzi wa daktari ambao hata hivyo hawatautoa kwa vyombo vya habari kwa kuwa huwa ni siri.

“Bado tunasubiria ripoti ya daktari na upelelezi unaendelea ila ripoti hiyo ni siri, si lazima apelekwe mahakamani kesho (leo) kwa kuwa bado upelelezi unaendelea,”alisema Kenyela.  Kanumba alifariki usiku wa kuamkia Jumamosi nyumbani kwake, Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam.  


Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kenyela, zilieleza kuwa kifo cha msanii huyo kilitokana na ugomvi uliotokea kati yake na mpenzi wake ndani ya nyumba yake.  Taarifa za kifo cha Kanumba zilianza kusambaa kuanzia saa 10.00 alfajiri na kuenea kwa kasi ambapo hadi kufikia saa moja asubuhi, mamia ya watu walikuwa wamejazana nyumbani kwa Kanumba kutaka kuthibitisha habari hizo.  Kadri muda ulivyozidi kusogea ndivyo idadi ya watu ilizidi kuongezeka nyumbani kwa msanii huyo ambaye amejizolea umaarufu mkubwa kutoka na filamu zake kuuzwa na kuonyeshwa katika vituo mbalimbali vya televisheni, ndani na nje ya nchi.

 Miongoni mwa watu waliomiminika kwa haraka nyumbani kwa Kanumba  ni wasanii wa fani mbalimbali nchini,  wanasiasa na viongozi mbalimbali wa Serikali  Chanzo cha kifo chake  Kwa mujibu wa maelezo ya mdogo wake aitwaye Seth ambaye alikuwapo eneo la tukio, alisema kaka yake alishinda nyumbani na baada ya kula chakula cha jioni, alimwambia wajiandae kutoka.  Seth alisema kuwa wakati Kanumba akiwa tayari amejiandaa, walisikia mlio wa gari likifunga breki nje ya nyumba. 

Alisema gari hilo lilikuwa limemleta mpenzi wa kaka yake msanii wa filamu, Lulu ambaye aliingia ndani na kwenda moja kwa moja chumbani kwa Kanumba.  Baada ya kuingia ndani, muda mfupi alisikia sauti zilizoashiria kuwa kulikuwa na ugomvi kati ya wapenzi hao.  “Ghafla ulizuka mzozo ndani na dakika chache baadaye, Lulu alitoka na kuja kuniambia kuwa Kanumba amedondoka baada ya kujigonga ukutani na kwamba yupo taabani hajitambui,” alisema Seth.

Alisema alipoingia chumbani, alimkuta kaka yake akiwa katika hali mbaya hivyo akaamua kumpigia simu daktari wake, ambaye alipofika na kuwashauri wampeleke haraka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupatiwa matibabu.  Seth alisema kabla ya kufika Muhimbili  walipitia Kituo cha Polisi cha Oysterbay kupatiwa Fomu ya matibabu (PF3).

Hata hivyo, baada ya polisi kupata maelezo ya awali ya ugomvi huo, walimshikilia Lulu kituoni hapo na kumwacha Seth akimpeleka Kanumba hospitali.  Alisema walipofikia Hospitali ya Muhimbili, madakati waligundua kuwa tayari Kanumba alishaaga dunia.  Awali Kamanda Kenyela akithibitisha kutokea kwa tukio hilo alisema Kanumba alikufariki kutokana na ugomvi uliotokea kati yake na rafiki yake wa kike Lulu.  http://www.mwananchi.co.tz/habari/4-habari-za-kitaifa/21887-hatima-ya-lulu-iko-mikononi-mwa-dpp

No comments:

Post a Comment