Thursday, April 14, 2011

Babu wa Loliondo anachemsha kilo 3 za mizizi

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema, Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambikile Mwaisapile, anachemsha kilo tatu za mizizi katika lita 60 za maji ili kupata dawa anayotumia kuwatibu watu katika Kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.

Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Hadji Mponda, amelieleza Bunge kuwa dawa ya Babu wa Loliondo ni salama lakini haijathibitika kama inatibu magonjwa anayosema.
Inadaiwa kuwa Mchungaji Mwaisapile anatoa kikombe cha dawa inayotibu magonjwa sugu ukiwemo Upungufu wa Kinga Mwilini (Ukimwi), Kisukari, saratani, na kifafa.

Dk. Mponda amewaeleza wabunge kuwa, serikali bado inafanya utafiti ili kufahamu kama ni kweli kikombe cha Babu kinatibu Ukimwi hivyo wananchi wawe na subira.

Ameyasema hayo bungeni mjini Dodoma wakati anajibu maswali ya Mbunge wa Viti Maalum, Maryam Msabaha aliyesema kuwa, waathirika wengi wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) vijijini hawana elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya ARV’s na wengi wao hawapati lishe bora je serikali ina mpango gani wa kuhakikisha misaada ya wafadhili inawafikia walengwa.

Waziri Mponda amekiri kuwa, waathirika wengi wenye VVU vijijini hawana elimu kuhusu matumizi ya ARV’s lakini Wizara kwa kushirikiana na wadau hutoa mafunzo kwa watoa huduma za tiba hiyo.

http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=16160

No comments:

Post a Comment